SEKTA BINAFSI KUPITIA PPP MGUU SAWA KATIKA JUHUDI ZA UZALISHAJI UMEME
Wadau wa maendeleo wameanza kuangazia kwa kina nafasi ya sekta binafsi kama nguzo muhimu ya kuziba pengo la rasilimali za serikali.
Hatua hiyo inakuja wakati Tanzania ikiweka malengo makubwa ya kufikia uzalishaji wa takribani megawati 70,000 za umeme ifikapo mwaka 2050.
Hii ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila.
Alikuwa akizungumza jijini Dar es Salaam huku akisema kuwa, uwezo wa serikali pekee kupitia mapato ya kodi na mikopo hautatosha kufanikisha malengo hayo makubwa ya nishati.
Badala yake, amesisitiza kuwa mustakabali wa utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo (FYDP IV) unategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa sekta binafsi, hasa katika uwekezaji wa miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme.
Aidha, juhudi hizo bado zinakabiliwa na changamoto za kisheria, hasa katika eneo la usafirishaji wa umeme ambapo baadhi ya aina za ubia haziruhusiwi ambapo Kafulila alifichua kuwa serikali imeanza majaribio ya miradi ya ubia kwa kushirikiana na TANESCO na kampuni binafsi, hatua inayolenga kupima ufanisi na kuweka msingi wa maboresho ya sera na sheria.
Kwa upande wake, Balozi Modest Mero ameonya kuwa mafanikio ya ushirikiano huo hayatategemea uwekezaji pekee, bali pia maadili na uwajibikaji wa wadau akisisitiza kuwa bila kuwa na mtazamo wa pamoja unaolenga manufaa ya taifa, kuna hatari ya maamuzi ya kiuchumi kuelekezwa kwenye faida binafsi badala ya ustawi wa wananchi.
Naye mtaalamu wa uchumi Dkt.Avit Mushi ameeleza kuwa sekta binafsi ina uwezo mkubwa wa kuongeza kasi ya maendeleo kutokana na ufanisi wake, lakini akatahadharisha kuwa mafanikio hayo yanahitaji pia mabadiliko ya fikra na uwajibikaji ndani ya taasisi.
mjadala huo unaonesha wazi kuwa safari ya kuelekea uchumi wa kisasa unaotegemea nishati ya uhakika si ya serikali pekee, bali ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano thabiti, sera rafiki, na uwajibikaji wa pande zote.
Post a Comment