SERIKALI YAANDAA MFUMO MPYA KUPATA VIONGOZI BORA
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora inaandaa utaratibu mpya wa upatikanaji wa viongozi kupitia mfumo maalum wa Leadership Competency Framework, lengo ni kuongeza msisitizo wa kuwajengea uwezo viongozi wapya na waliopo ili nafasi za uongozi zisigeuke majaribio.
Akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Open University of Tanzania (OUT) yaliyofanyika katika ukumbi wa shule ya uongozi Mwalimu Nyerere Kibaha , Machi 11, 2026, Xavier Mrope, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais–Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, ameeleza kutokana na dunia kuwa ya ushindani na matumizi ya mifumo ya tathmini ya uongozi, taifa linahitaji viongozi walioandaliwa.
Hata hivyo, Serikali inaendeleza utamaduni wa kuchuja na kupima uwezo wa viongozi si kwa kuangalia vyeti pekee bali pia haiba ya uongozi, uwezo wa kufanya maamuzi, maadili, usimamizi wa migogoro na uwezo wa kuongoza mabadiliko.
Akizungumzia matarajio ya mafunzo hayo, Kaimu Makamu Mkuu wa OUT, Harieth Hellar-Kihampa, amesema mafunzo hayo ya siku nne yanafanyika kuanzia Machi 11 hadi 14, 2026 yakihusisha washiriki 75, na yanalenga kuwajengea uwezo wakiwemo viongozi wapya, wakuu wa idara ili kuongeza ufanisi kazini.
Nae Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa OUT anayeshughulikia Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa, Paul Kwaba, ameeleza chuo hicho kwa sasa kina vituo 26 katika mikoa ya Tanzania Bara vinavyotoa huduma mbalimbali huku mpango ukiwa kufikia ngazi ya wilaya.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Leadership School, Marcellina Chijoriga, Meneja Taaluma John Baitan analeza shule hiyo hutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu ikiwemo uzalendo, uongozi wa kimkakati, utawala bora, uadilifu, usimamizi wa miradi, falsafa ya ukombozi pamoja na ubunifu na mabadiliko ya kidijitali ili kuongeza tija na kupanua huduma kwa Watanzania.
.jpeg)
Post a Comment