SHILINGI BILIONI 2 ZATOLEWA NA REA KUENDELEZA MRADI WA IJANGALA, MAKETE


Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini-REA imetoa shilingi bilioni 2 ili kuendeleza mradi wa kufufua umeme wa Ijangala, uliopo wilayani Makete, Mkoani Njombe.

Tayari, mradi huo umeshaanza kufanya kazi tangu mwaka 2025 na unaingiza kilowati 360 za umeme katika gridi ya Taifa ya umeme.

Kufuatia mafanikio hayo, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeipongeza REA kwa kujenga mazingira wezeshi kwa sekta binafsi nchini iliyowezesha wananchi waliopo maeneo ya Vijijini na pembezoni mwa miji kupata huduma bora ya nishati ya umeme kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. 

TEF imesifu hatua hiyo baada ya kutembelea mradi huo wa umeme wa Ijangala (Ijangala Mini Hydropower Plant 360 kW) uliopo Wilaya ya Makete.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ameisifu  REA kwa juhudi zake za kuweka kiasi kikubwa cha fedha shilingi bilioni 2 za kuendeleza na kutekeleza mradi huo ambao umesaidia kuongeza ubora na upatikanaji wa umeme mkoani Njombe. 

Aidha, wahariri wa habari wameelezea kuridhishwa na mradi huo wa Ijangala, wakisema unasaidia kuchochea uchumi wa wananchi wa Makete na mkoa wa Njombe kwa ujumla.

Naye, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yessaya amesema REA  imekuwa ikifadhili miradi ya uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme vijijini hususani inayotekelezwa na taasisi mbalimbali za Serikali na za watu binafsi kwa kutoa ruzuku pamoja na mikopo ya masharti nafuu. 

Mradi wa Ijangala unatajwa kumeleta faida mbalimbali ikiwemo kuongezeka kiwango cha umeme unaozalishwa nchini, kuimarisha, hali ya ubora wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na kusaidia kupunguza hewa ya ukaa ambayo ingezalishwa kwa kutumia vyanzo vingine vya umeme. 

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi wa umeme Ijangala, Daudi Sanga, amesema kwa kiasi kikubwa mradi huo umefadhiliwa na REA na wadau wengine wa maendeleo na mradi huo wa Ijangala kwa sasa unazalisha kilowati 360 zinazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa







No comments