TANZANIA YAJIVUNIA KUTOA MAFUNZO YA MAABARA YA KIBAILOJIA KWA NCHI WANACHAMA 14
Serikali ya Tanzania kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii chini ya Wizara ya Afya imeendelea kujivunia utoaji wa mafunzo ya Kikanda ya Uteuzi, Ufungaji, Matengenezo na Udhibiti Ubora wa Makabati ya Usalama wa Kibailojia (BSCs) kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Hayo yamesemwa Machi 11, 2026 jijini Dar es Salaam na mmoja ya wakufunzi wa kozi hiyo, Mhandisi wa Vifaa tiba Sylidion Kaguwila wa Maabara ya Taifa wakati wa mafunzo hayo, ambapo amesema, mafunzo hayo ya siku kumi yamekuwa na msaada kwa washiriki ambao huko walipotokea baadhi yao walikuwa hawajawahi kuona makabati hayo ya kibailojia.
“Walipofika siku ya kwanza na leo ni vitu viwili tofauti, hii inatokana na kwamba, mafunzo haya wanafanyika kwa vitendo, hali inayochangia kuelewa kwa ufasaha pamoja kwamba, baadhi yao hawaongei Kiswahili wala kingereza, kwani wametokea kwenye nchi zinazozungumza Kifaransa na Lugha zingine” amesema Mhandisi Kaguwila.
Kwa upande wake mmoja ya wapatiwa mafunzo, Mhandisi Joyce Aura kutoka nchini Kenya katika Hospitali ya Kaunti ya Kisumo, amesema kuwa, mafunzo hayo yamekuwa na msaada mkubwa kwa kuwa yatamsaidia kwenye utendaji kazi wake lakini pia kutoa elimu sehemu ya kazi kwa wenzake ambao hawakubahatika kuhudhuria mafunzo hayo.
Naye Mhandisi Emmanuel Ian, kutoka nchini Uganda, anayehudhuria kozi hiyo kwa mara ya kwanza, amekiri kuwa Afrika ina uhaba wa wataalamu wenye uwezo wa kufanya matengenezo kinga ya Makabati ya usalama yaani biological safety cabinet hivyo yaye kama mnufaika atakaporejea nchini kwake baada ya mafunzo atahakikisha kuwa ujuzi huo alioupata anawapatia na wataalamu wengine.
Kwa upande wake Mhandisi Salome Kumba muandaaji wa mafunzo kutoka Maabara ya taifa ya afya ya jamii amesema, hii ni mara ya pili kwa wataalamu kutoka inchi za ukanda wa afrika mashariki kupata mafunzo hayo katika kituo hicho kwa ngazi ya kwanza.
Aidha ameongeza kwa kusema kuwa mafunzo hayo ni nguzo muhimu kwa kuboresha usalama, ubora wa matokeo na ufanisi wa huduma za maabara barani Afrika. Uwekezaji katika mafunzo haya huchangia moja kwa moja katika uimarishaji wa mifumo ya afya na utafiti.



Post a Comment