TASAC WATOA MSAADA KWA WATU WENYE UHITAJI MAALUM

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo, tarehe 12 Machi 2026, limetekeleza jukumu lake la uwajibikaji kwa jamii kwa kutembelea na kutoa msaada wa chakula pamoja na vifaa mbalimbali kwa watu wenye uhitaji katika kituo cha kulea watoto wenye mtindio wa ubongo cha Dorcas Home Care Initiative kilichopo Madale, pamoja na Kanisa la Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo iliongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Shirika Bw. Hamid Mbegu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu akiongozana na baadhi ya watumishi wa Shirika.

Wakiwa katika ziara hiyo, ujumbe wa TASAC ulikabidhi msaada wa chakula na vifaa mbalimbali, sambamba na kufanya mazungumzo na walezi wa kituo hicho pamoja na viongozi wa Kanisa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI). 

Watumishi hao walipata fursa ya kujionea mazingira na changamoto zinazowakabili watoto wenye uhitaji pamoja na wagonjwa, huku wakisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kijamii na upendo kwa makundi yenye uhitaji maalum.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada huo, Bw. Mbegu alieleza kuwa TASAC inaamini katika dhana ya uwajibikaji kwa jamii, na kwamba Shirika linatimiza wajibu wake kwa kushiriki moja kwa moja katika kuonesha upendo na mshikamano kwa jamii, hususan katika kipindi hiki cha Kwaresma na Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. 

Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Kituo cha kulea watoto wenye mahitaji maalum, Bi. Rehema Semfukwe; Mwinjilisti wa KKKT Muhimbili, Bi. Rachel Maoni; pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii wa MOI, Bi. Theresia Jacob, walitoa shukrani kwa TASAC kwa msaada huo. 

Viongozi hao waliipongeza TASAC kwa kuonesha moyo wa kujali jamii na kutoa wito kwa wadau wengine na jamii kwa ujumla kuendelea kutoa msaada kwa makundi yenye uhitaji maalum.

Aidha, walisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu afya ya uzazi, wakieleza kuwa elimu hiyo inaweza kusaidia kupunguza changamoto zinazochangia kuzaliwa kwa watoto wenye mtindio wa ubongo pamoja na magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika.

No comments