TASAC YAONGEZA NGUVU KUDHIBITI USALAMA WA WAVUVI MKOA WA MARA
Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Mara, Mhandisi Hezroni Lusangija, amesema kuwa taasisi hiyo imeongeza juhudi za ukaguzi na ufuatiliaji katika shughuli za uvuvi ili kuhakikisha wavuvi wanazingatia kikamilifu kanuni za usalama wanapokuwa majini mkoani humo.
Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika na kuimarisha usalama wa wavuvi, hususan katika kipindi hiki cha changamoto za hali ya hewa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Lusangija, TASAC imejipanga kuendesha ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya uvuvi na mialo, sambamba na kuendelea kutoa elimu ya usalama kwa wavuvi ili kujenga uelewa na kuwahamasisha kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa vya uokozi.
Hatua hiyo imepokelewa vyema na viongozi wa serikali za mitaa katika vijiji vya Mkengwa, Kibuyi, Kinesi na maeneo ya jirani wilayani Rorya, ambao wameahidi kushirikiana na TASAC kudhibiti vitendo vya uzembe vinavyofanywa na baadhi ya wavuvi.
Viongozi hao wameeleza kuwa miongoni mwa changamoto kubwa ni tabia ya baadhi ya wavuvi kutovaa majaketi ya uokozi wanapokuwa majini, hali inayohatarisha maisha yao.
Aidha, wameahidi kuimarisha usimamizi katika maeneo ya mialo kwa kuchukua hatua kali dhidi ya wavuvi watakaokiuka taratibu za usalama, huku wakisisitiza kuwa watahakikisha elimu iliyotolewa na TASAC inawafikia wavuvi wote katika maeneo yao.
Mafunzo hayo ya matumizi sahihi ya vifaa vya uokozi yametolewa na TASAC kwa kushirikiana na Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Rorya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usalama na ustawi wa wavuvi mkoani Mara.
Post a Comment