WAZIRI DKT. GWAJIMA AIPAMBA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA UZINDUZI WA MRADI WA TSH BILIONI 262


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe.  Dkt. Dorothy Gwajima , amezindua Mradi wa PAMOJA (Project for Advancing Gender Equality in Tanzania) wenye thamani ya shilingi bilioni 262 unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano na Benki ya Dunia.

Uzinduzi huo umefanyika katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani yaliyofanyika tarehe 8 Machi 2026 mkoani Geita, yenye kaulimbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira ya 2050.” ambapo Waziri  Dkt. Gwajima alikuwa mgeni rasmi katika kilele hicho

Mradi huo unalenga kukuza usawa wa kijinsia kwa kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake, kuimarisha juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia pamoja na kuboresha huduma kwa manusura wa vitendo hivyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Gwajima amesema kuwa uwekezaji kwa wanawake na wasichana ni mkakati muhimu katika kujenga jamii yenye usawa na ustawi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. 

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha usawa wa kijinsia kwa kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wanawake.

Aidha, Dkt. Gwajima amewahimiza walengwa wa mradi ambao ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa upande wa Tanzania Bara pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto Zanzibar kuupokea kwa mikono miwili  kutoa ushirikiano unaostahili na kuutunza ili uweze kuleta maendeleo endelevu katika jamii.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu , amesema kuwa mradi huo utatekelezwa katika mikoa 10 na halmashauri 40 za Tanzania Bara na Zanzibar. 

Alifafanua kuwa miongoni mwa malengo ya mradi huo ni kuwezesha mitaji kwa wanawake wajasiriamali, kuimarisha programu za malezi na makuzi ya watoto, pamoja na kujenga jumla ya vituo 200 vya huduma hizo; vituo 184 vikiwa Tanzania Bara na 16 vikiwa Zanzibar.

Aidha, ameeleza kuwa mradi huo pia unalenga kubadili mitazamo hasi ya jamii inayokwamisha maendeleo na ustawi wa wanawake na watoto, pamoja na kujenga uwezo wa wanawake na wataalamu mbalimbali ili kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa malengo ya mradi. Vilevile, mradi unatambua umuhimu wa ushirikishwaji wa wanaume katika juhudi za kufikia matokeo chanya kwa haraka.

Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Aun Ali Rahman , ameipongeza Tanzania kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuimarisha usawa wa kijinsia. Amesema Benki ya Dunia inaona jitihada hizo kuwa muhimu katika kukuza maendeleo jumuishi ya jamii. 

Aidha, ameahidi kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuimarisha ustawi wa wanawake, watoto na jamii kwa ujumla.









No comments