BAJETI YA WIZARA YA NISHATI 2026/2027 YAGUSA MAENDELEO KWA ASILIMIA 97.5
Waziri wa Nishati,Deogratius Ndejembi ameomba kuidhinishiwa na Bunge Sh. trilioni 2.53 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2026/27, ambapo sh. trilioni 2.46 sawa na asilimia 97.5 ya bajeti yote imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa mwaka 2026/2027 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma Ndejembi ameainisha vipaumbele vya utekelezaji wa bajeti hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha uwepo wa nishati ya kutosha na endelevu.
Ndejembi amesema katika mwaka 2026/2027 Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea kuiimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na kuunganisha mikoa ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara kwenye Gridi ya Taifa.
Kipaumbele kingine ni kuongeza kasi ya kuunganisha umeme kwa wananchi ili kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii na kutekeleza mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa (Gridi Imara) ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika, sambamba na kufanya matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Aidha katika mwaka 2026/2027 Wizara itaendelea na usambazaji wa umeme katika vitongoji na maeneo ya shughuli za kiuchumi na kijamii kama maeneo ya migodi, kilimo, viwanda, shule, pampu za maji na vituo vya afya na kuwezesha ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini ili kuimarisha upatikanaji wa nishati safi na salama.
Amesema pia Serikali itaendelea kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na Mpango Mahususi wa Taifa wa Nishati (2025-2030) huku mkazo ukielekezwa katika kuziwezesha kaya na taasisi zinazohudumia chakula kwa zaidi ya watu 100 kwa siku.
Kwa upande wa Mafuta na Gesi Asilia, Ndejembi amesema Serikali itaendeleza miradi ya utafutaji na uzalishaji ikiwemo mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika ( LNG), mradi wa uendelezaji wa gesi asilia eneo la Ntorya katika Kitalu cha Ruvuma na miradi ya kielelezo na kimkakati ya utafutaji mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara na Mnazi Bay















Post a Comment