BILIONI 13.97 KUPELEKA VIFAA VYA MAABARA SHULE ZA SEKONDARI 672 NCHINI
Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuimarisha elimu ya sayansi nchini kupitia uwekezaji mkubwa katika vifaa na miundombinu ya maabara kwa shule za sekondari.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo Aprili 23, 2026 na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Elimu), Dkt. Festo Dugange kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mwantatu Mbarak Khamis, aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani kuhakikisha Shule za Sekondari zinaondokana na upungufu wa vifaa vya Maabara.
Katika majibu yake ya awali, Dkt. Dugange ameeleza kuwa tayari Serikali imetumia Shilingi Bilioni 3.51 katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kununua na kusambaza kemikali na vifaa vya maabara kwa shule za sekondari 231, huku mchakato ukiendelea wa ununuzi wa vifaa vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 13.97 kwa shule 672 zaidi.
Akijibu maswali ya nyongeza, Naibu Waziri ameeleza kuwa Serikali imeweka kipaumbele kikubwa katika ujenzi wa shule za sayansi za mikoa, ambapo shule 26 zimejengwa kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 4.6 kila moja, zikiwa na maabara kamili pamoja na wataalamu wake ili kuhakikisha masomo ya sayansi yanafundishwa kwa ufanisi mkubwa.
Aidha, ametoa maelekezo mahususi kwa utekelezaji, akibainisha kuwa Serikali ina mpango madhubuti wa kukamilisha maabara ambazo hazijakamilika, kujenga mpya pale penye uhitaji, na kupeleka vifaa pamoja na wataalamu wake.
Ameongeza kuwa mpango kabambe wa kuboresha miundombinu ya elimu ya sayansi na mafunzo ya amali uko katika hatua za mwisho, ukilenga kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kuongeza umahiri katika sayansi na teknolojia.

Post a Comment