Dkt. Ashatu Kijaji Awapongeza Askari wa Uhifadhi wa TFS kwa Kulinda Shamba la Miti Silayo



Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb),amewapongeza askari wa uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanaofanya kazi katika Shamba la Miti Silayo, wilayani Chato, kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda na kuhifadhi shamba hilo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.



Dkt. Kijaji ametoa pongezi hizo leo, Aprili 16, 2026, alipokuwa katika ziara ya kukagua shamba hilo, akibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana yametokana na ari ya kujituma, mshikamano na umoja wa askari hao katika kuhakikisha shamba linabaki katika hali bora na ya kuridhisha.



“Niwapongeze sana askari wetu mnaofanya kazi nzuri sana huku uwandani. Kazi yenu ni njema mno, tunawapongeza sana. Na pongezi hizi hazitoki kwangu tu, bali zinatoka moja kwa moja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amenituma kuwafikishia pongezi hizi,” amesema Dkt. Kijaji.



Aidha, ameongeza kuwa kazi wanayoifanya askari hao ni muhimu sana kwani inachangia moja kwa moja katika kulinda mazingira, hasa ikizingatiwa kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi hujitokeza pale ambapo juhudi za uhifadhi hazijazingatiwa ipasavyo.



Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, kabla ya kumkaribisha Waziri kuzungumza, amesema kuwa Shamba la Miti Silayo ni la pili kwa ukubwa nchini baada ya Shamba la Sao Hill, jambo linalolifanya kuwa miongoni mwa fursa kubwa za kiuchumi kwa taifa.


Naye Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi, Bi. Zainabu Bungwa, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi Dkt. Dos Santos Silayo, amesema kuwa Shamba la Miti Silayo ni hazina kubwa kwa taifa kwani limekuwa likisaidia jamii inayolizunguka katika nyanja mbalimbali, ikiwemo utoaji wa misaada mbalimbali katika jamii. 


Baada ya kutembelea Shamba la Miti Silayo, Dkt. Kijaji alipata fursa ya kukutana na askari wa uhifadhi kutoka TFS na TANAPA wa eneo hilo, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji katika maeneo yao.











No comments