DKT. MNYEPE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 13 WA AMANI, ULINZI, USALAMA NA SERA ZA MAMBO YA NJE EAC
Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe ameongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 13 wa Pamoja wa Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri wa Ushirikiano katika Ulinzi, Amani na Usalama na Baraza la Kisekta la Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Nairobi, Kenya, Aprili Mosi 2026.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa ni pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa Maamuzi yaliyopita ya Baraza hilo, hatua iliyofikiwa katika uandaaji wa Mfumo Jumuishi wa Tahadhari ya Mapema, kupitia Rasimu ya Mpango Mkakati wa Ushirishwaji wa Wanawake katika amani, ulinzi na usalama wa EAC, kupitia Mpango Mkakati wa Ushirishwaji wa Asasi zisizo za kiserikali katika uzuiaji, usimamizi na utatuzi wa migogoro katika EAC.
Aidha, Makatibu Wakuu wamefanya mapitio ya Utekelezaji wa Programu ya uelimishaji wa Jamii zinazoishi mipakani kuhusu ujirani mwema na masuala ya usimamizi wa mipaka.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Said Shaib Mussa na Dkt. Maduhu Kazi, mtawalia wameshiriki Mkutano huo kwa niaba ya Makatibu Wakuu wao.
Mkutano wa Makatibu umepitisha Ripoti ya waliyojadili ambayo itawasilishwa katika Mkutano wa Ngazi ya Mawaziri ambao Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahamoud Thabit Kombo ataongoza Ujumbe wa Tanzania kwa kushirikiana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Post a Comment