KAMATI YA UTALII, BIASHARA NA KILIMO YATAKA MAMLAKA YA VIPIMO ZANZIBAR IFIKIE VIWANGO VYA WMA BARA


Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, imekiri hi kuvutiwa na utendaji kazi wa Wakala wa Vipimo-WMA, Tanzania Bara na kuahidi kuweka mikakati ya makusudi itakayoisaidia Mamlaka inayosimamia vipimo Zanzibar-ZAWEMA, kutekeleza majukumu yake kwa kiwango hicho au zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara ya mafunzo katika Kituo cha Vipimo Misugusugu, mkoani Pwani, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Mohammed Ali Suleiman, amesema Wakala wa Vipimo upande wa Tanzania Bara wamepiga hatua kubwa kiutendaji hivyo kuna kila sababu ya Zanzibar kufuata mfano huo.

Dkt. Suleiman, amesema Kamati yake itaishauri Wizara ya Biashara ambayo ndiyo inayoisimamia Mamlaka ya Vipimo Zanzibar, kuweka mikakati ya makusudi ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, wataishauri Serikali kuhakikisha ZAWEMA, ambayo ndiyo Mamlaka ya Vipimo kwa upande wa Zanzibar, kwanza inakuwa Mamlaka huru lakini pia ipate mitambo ya kisasa ya uhakiki vipimo na pia ishirikiane kwa ukaribu na WMA ili iweze kutekeleza majukumu yote kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, amesema anaamini kuwa kupitia ziara hiyo ya mafunzo kwa Kamati kutoka Baraza la Wawakilishi, jukumu la uhakiki na ukaguzi wa vipimo linaenda kuwa bora zaidi kwa pande zote mbili; Zanzibar na Tanzania Bara.

Kuhusu ushirikiano uliopo kati ya WMA na ZAWEMA, Mtendaji Mkuu huyo amesema Taasisi hizo mbili zilikwishasaini Hati ya Ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kushiriki kwenye mikutano ya kikanda na kimataifa pamoja na katika kaguzi za vipimo hususan katika bidhaa zilizofungashwa.

Kwa sasa, Wakala wa Vipimo Tanzania ndiye Mwenyekiti wa Jukwaa la Kikanda linaloratibu masuala ya kivipimo kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADCMEL







.

No comments