MORCASE: POLISI PWANI WAKAMATA WATUHUMIWA 206 WA DAWA ZA KULEVYA, MAGENDO NA MAKOSA MENGINE

 


Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa 206 kwa makosa mbalimbali ya jinai katika operesheni na misako iliyofanyika kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema operesheni hizo zinalenga kuimarisha usalama wa raia na mali zao.


Morcase ameeleza kati ya waliokamatwa, watuhumiwa 89 wanahusishwa na biashara na matumizi ya dawa za kulevya. 


Katika operesheni hizo, polisi walikamata puli 59 za bangi, kete 2,361, misokoto sita, pakiti 150 za bangi zenye uzito wa kilo 2.8 na bunda 95 za mirungi zenye uzito wa kilo 95 zilizokuwa zinasafirishwa kwa pikipiki.


Aidha, watu 35 walikamatwa kwa kutengeneza na kusambaza pombe haramu ya moshi, ambapo lita 172 za pombe hiyo pamoja na mitambo minne ya kutengenezea zilinaswa. 


Polisi pia waliwakamata watuhumiwa tisa waliokuwa wakiingiza nchini mafuta ya kula yenye ujazo wa lita 1,520 kupitia bandari bubu za Bagamoyo wakikwepa kulipa ushuru wa Serikali.


Kwa upande wa usalama barabarani, madereva wanane walifungiwa leseni huku madereva 71 wakifikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.


Vilevile, makosa 20,380 ya barabarani yalibainika na wahusika kutozwa faini pamoja na kupewa elimu ya kuzingatia sheria hizo.

No comments