MAFUNZO HUDUMA ZA DHARURA YAIMARISHA HUDUMA HOSPITALI YA WILAYA KIBONDO



Huduma za dharura na wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo zimepata msukumo mpya kufuatia mafunzo maalum ya wataalam kutoka Serikali, hatua inayotarajiwa kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya mkoani Kigoma.


Hospitali ya Wilaya ya Kibondo imepiga hatua mpya katika kuboresha huduma zake baada ya watumishi wa Hospitali hiyo kupatiwa mafunzo ya utoaji wa huduma za dharura na mahututi yaliyoratibiwa na wataalam kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu– TAMISEMI.


Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Cornely Livin, amesema hayo Aprili 21, 2026 wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo


Amesema, mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yameongeza uelewa na ufanisi wa watumishi ili kukabiliana na hali za dharura kama ajali na magonjwa ya ghafla kwani awali kulikuwa na changamoto ya mpangilio hafifu wa huduma, licha ya uwepo wa miundombinu na baadhi ya mafunzo ya awali.


Dkt. Livin ameongeza kuwa, kupitia mafunzo hayo, hospitali imepata mwongozo sahihi wa matumizi ya vifaa tiba, upangaji wa huduma na uboreshaji wa mfumo wa utoaji huduma kwa wagonjwa mahututi.


Amesisitiza, umuhimu wa mafunzo hayo kuendelea kutolewa mara kwa mara ili kuwajengea uwezo watumishi wapya na kuimarisha ubora wa huduma kwa jamii.


Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Dharura na Ajali, Dkt. Ezra Marwa, amesema jengo la huduma za dharura na mahututi lililoanza kutumika mwaka 2023 limekuwa na mchango mkubwa wa kuboresha huduma hizo, na mafunzo hayo yameongeza ufanisi zaidi kwa matumizi yake.


Kwa upande wake Afisa Muuguzi wa hospitali hiyo, Bw. Lazaro Mlobela, amesema mafunzo hayo yameleta mabadiliko chanya kwa watumishi, hasa katika upangaji wa vifaa, usafi wa vifaa tiba na matumizi sahihi ya mashine, hatua inayosaidia kuongeza ubora wa huduma kwa wagonjwa.


Mafunzo hayo yameiwezesha Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kuimarisha huduma zake za dharura na mahututi, huku yakitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za Serikali za kupunguza vifo vinavyotokana na dharura na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika sekta ya afya nchini.

















No comments