MFUMO WA UKUSANYAJI TAARIFA ZA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU (PAIS) WAHARAKISHA MALIPO YA KIFUTA JASHO KWA WANANCHI



Serikali imeanza kutumia Mfumo wa kielektroniki wa (Problem Animal Information System (PAIS), kurahisisha ukusanyaji na uwasilishaji wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu wanaohatarisha maisha na kuharibu mali nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara.



Hayo yamebainishwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), katika kikao cha 16 Mkutano wa tatu wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akijibu swali la Mhe Mary Daniel Surati (Mb.) aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kutoa fidia kwa wakati kwa wananchi walioathiriwa na Wanyamapori Wilayani humo



Mhe Chande amebainisha kuwa mfumo huo tayari umeanza kufanya kazi na umesaidia  kuongeza kasi ya uchakataji na uhakiki wa taarifa zinazowasilishwa, kuwezesha malipo ya kifuta jasho na machozi kufanyika kwa wakati na kupunguza udanganyifu wa taarifa zinazowasilishwa.


Awali Mhe. Chande alibainisha kuwa, Serikali imekuwa ikilipa kifuta jasho na kifuta machozi kama mkono wa pole au faraja kwa wananchi wanaopata madhara kwa lengo la kuimarisha mtazamo chanya kwa wananchi juu ya shughuli za uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori nchini na kusisitiza kuwa malipo hayo yamekuwa yakifanyika kwa mujibu wa kanuni za kifuta Jasho za Mwaka 2011 na Marekebisho yake ya Mwaka 2024

No comments