NEEMA MSITHA AZINDUA RASMI MFUMO WA KIDIGITALI WA KAMISHENI YA NGUMI ZA KULIPWA TANZANIA
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa, Bi. Neema Msitha, leo tarehe 16 Aprili 2026 amezindua rasmi mfumo mpya wa kidigitali wa TPBRC, mfumo unaotarajiwa kubadilisha kwa kiwango kikubwa namna wadau wa ngumi wanavyopata huduma na kusimamiwa.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali na wadau wa michezo kuhimiza matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi, uwazi na utunzaji wa takwimu.
Mfumo huu mpya unapatikana kupitia tovuti ya Kamisheni, tpbrc.or.tz, na umeundwa mahsusi kurahisisha huduma mbalimbali muhimu kwa wanamichezo wa ngumi za kulipwa pamoja na wadau wengine.
Kupitia mfumo huo, watumiaji wataweza kuomba vibali vya safari, kusajili gym, kusajili makocha wa ngumi, kusajili mabondia, pamoja na kuomba vibali vya malumbano kwa njia rahisi, haraka na salama.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bi. Msitha amesema mfumo huo ni mapinduzi makubwa katika tasnia ya ngumi za kulipwa nchini Tanzania, hasa katika kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kupunguza urasimu.
Mfumo huo pia utawezesha kumtambua bondia popote alipo, kubaini anafanya mazoezi katika gym gani, pamoja na kurahisisha ufuatiliaji wa kumbukumbu za mafunzo na malumbano yake.
Aidha, TPBRC sasa itaweza kufuatilia, kuhifadhi na kusimamia taarifa zote kwa usalama wa hali ya juu, jambo litakaloongeza uwazi, ufanisi na uaminifu kwa wadau wa mchezo huo.





Post a Comment