MGOGORO WA NYUMBA YA URITHI PLOT NAMBA 6, MTAA WA NGARENARO, KATA YA BAGARA, DC KAGANDA ATATUA.


Katika jitihada za kuhakikisha migogoro ya wananchi inatatuliwa kwa njia ya amani na ustawi wa jamii kuimarika, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuela Kaganda, amekutana na wanafamilia wenye mgogoro unaohusisha uuzaji wa nyumba ya urithi iliyopo Mtaa wa Ngarenaro, Kata ya Bagara wilayani humo.


Katika kikao hicho, ilibainika kuwa baadhi ya wanafamilia walikubaliana nyumba hiyo iuzwe na fedha zitokanazo na mauzo zigawanywe kwa usawa huku, mmoja wa wanafamilia alionesha kutokubaliana na uamuzi huo, hali iliyochangia kuibuka kwa mgogoro huo mkubwa dhidio yao.


Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mhe. Kaganda alitoa ushauri kuwa nyumba hiyo iuzwe na mapato yagawanywe kwa usawa miongoni mwa wanafamilia wote huku akisisitiza kuwa wanafamilia wasiokuwa na uwezo watafutiwe makazi mbadala kwa ajili ya kuendelea na maisha yao.


Aidha Kwa upande wa mwanandugu aliyekataa kupokea fedha zake, Mhe. Kaganda alipendekeza fedha zake zihifadhiwe benki kwa usalama hadi pale atakapokuwa tayari kuzipokea.


Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Wilaya aliwakumbusha kuwa migogoro ya kifamilia huathiri maendeleo, na kuongeza mifarakano, na hata kuhatarisha usalama wa wanafamilia kutokana na migogoro ya mali za urithi.


Alimalizia kwa kuwasisitiza kuwa wanafamilia hao wanapaswa kuweka kando tofauti zao, kudumisha umoja na mshikamano, na kushirikiana katika kujenga maendeleo ya pamoja kama familia.




No comments