RAIS DKT. MWINYI ASISITIZA SMZ KUIMARISHA HUDUMA NA ELIMU KUHUSU USONJI



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Usonji kwa watoto ni changamoto kubwa ya kijamii inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau mbalimbali katika kuwatambua na kuwasaidia watoto wanaoathirika.



Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 20 Aprili 2026, alipokutana na viongozi wa Lukiza Autism Foundation waliomtembelea Ikulu Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha na kueleza shughuli za taasisi yao.



Amesema changamoto ya Usonji inachangiwa na uelewa mdogo wa jamii pamoja na uhaba wa wataalamu wa fani hiyo, hivyo Serikali inaendelea kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha wataalamu wanapatikana na elimu inaongezwa kwa wananchi.



Aidha, ameielekeza Wizara ya Afya kushirikiana na wataalamu hao ili kuimarisha utambuzi wa mapema na huduma kwa watoto wenye Usonji, pamoja na kuanzisha programu za uelimishaji mashuleni ili kuongeza uelewa wa jamii.



Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za taasisi mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha ya watoto wenye Usonji na kuhakikisha huduma bora zinapatikana.



Kwa upande wake, Mtendaji Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Lukiza Autism Foundation, Bi. Hilda Nkabe, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa wataalamu na vituo maalum, huku wakiahidi kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuanzia familia hadi mashuleni ili kuongeza uelewa na utambuzi wa mapema.



Ameongeza kuwa takribani watoto milioni 2 nchini Tanzania wanaonyesha dalili za Usonji, huku kati ya watoto 14,000 hadi 20,000 wakihitaji utambuzi na uangalizi maalum.








No comments