SERIKALI IMETENGA SHILINGI BILIONI 1.8 KWA AJILI YA UJENZI WA OFISI ZA TANAPA KANDA YA MAGHARIBI


Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za shirika hilo katika Ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Magharibi ili kuwa na mwitikio wa haraka dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu wasisababishe madhara kwa wananchi wanaopakana na hifadhi hiyo. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma katika kikao cha tisa cha mkutano wa tatu wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda Mjini Mhe. Ester Amos Bulaya aliyetaka kufahamu lini ujenzi wa Makao Makuu ya TANAPA Kanda ya Magharibi utaanza katika jimbo hilo, na kusisitiza kuwa taratibu zote za maandalizi za kuanza ujenzi wa mradi huo zikiwemo usanifu wa majengo na gharama za ujenzi wa mradi huo zimekamilika.  

“Ni kweli Serikali imetenga eneo lenye ukubwa wa Ekari 41.13 katika eneo la Kunzugu Kata ya Balili, Bunda Mjini kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Magharibi ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania” alisema Mhe. Chande

Awali, Mhe. Chande alifafanua kuwa, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linasimamia Hifadhi za Taifa 21 zilizogawanywa katika Kanda nne (4) ikiwemo Kanda ya Magharibi ambayo Makao Makuu yake yapo Mji Mdogo wa Bunda, Mkoani Mara ambapo kanda hiyo inajumuisha Hifadhi za Taifa zipatazo tisa (9) zinazosimamiwa na TANAPA ikiwemo Hifadhi za Taifa Serengeti, Visiwa vya Saanane na Rubondo, Burigi-Chato, Milima Mahale, Ibanda-Kyerwa, Rumanyika-Karagwe, Mto Ugalla na Gombe.

No comments