WCF YASISITIZA ELIMU YA FIDIA, YAZINDUA MFUMO WA KIDIJITALI
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi-WCF- umeeleza dhamira yake ya kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi, huku ukitangaza maboresho ya huduma zake kupitia mifumo ya kidijitali ili kuongeza uwazi na ufanisi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt John Mduma, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika Aprili 16, 2026 jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mduma amesema WCF ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria, ikiwa na jukumu la kushughulikia fidia kwa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi wanaopata ajali, kuugua au kufariki kutokana na kazi wanazofanya.
Amefafanua kuwa majukumu ya mfuko huo ni pamoja na kusajili waajiri, kukusanya michango, kulipa fidia, kufanya tathmini ya mazingira ya kazi pamoja na kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Aidha, WCF hutoa mafao mbalimbali ikiwemo huduma za matibabu, fidia ya ulemavu wa muda na kudumu, malipo kwa wategemezi wa mfanyakazi aliyefariki, pamoja na msaada wa mazishi.
Katika hatua ya kuboresha huduma, Dkt. Mduma amesema zaidi ya asilimia 95 ya huduma za WCF zinapatikana kwa njia ya mtandao, jambo lililosaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Mfuko huo umezindua mfumo mpya wa kidijitali utakaowawezesha wafanyakazi kufuatilia michango yao, madai ya fidia pamoja na kuwasiliana moja kwa moja na WCF kupitia simu zao za mkononi.
Naye, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ameupongeza mfuko huo wa WCF kwa kuendelea kuinga mkono TEF katika mikutano yake mbalimbali na kusisitiza ushirikiano huo uendelee pia hata kwa taasisi nyingine.

.jpeg)
.jpeg)

Post a Comment