SERIKALI NA TDCU KUZITATUA CHANGAMOTO ZA KIWANDA CHA MAZIWA TANGA

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Bodi ya Maziwa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Chama cha Ushirika wa Wazalishaji Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU ) inaendelea na utatuzi wa changamoto za Kiwanda cha Kusindika Maziwa cha Tanga (Tanga Fresh ) ambacho kina uwezo wa kusindika maziwa lita 120,000 kwa siku. 

Hayo yameelezwa leo Aprili 13, 2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM) Mhe. Timotheo Paul Mnzava wakati wa Kipindi cha Maswali na Majibu cha Bunge la Kumi na Tatu (13), Mkutano wa Tatu (3), Kikao cha Saba(7).

Swali hilo lilihoji juu ya mkakati wa serikali wa kuwasaidia wafugaji wa Korogwe Vijijini na Mkoa wa Tanga kwa ujumla kupata soko na bei ya uhakika ya maziwa, ambapo Naibu Waziri Mhe. Kamani amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maziwa zikiwemo taasisi za fedha imeshaanza kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kiwanda hicho kiendelee na uzalishaji.

“Mheshimiwa Mwenyekiti Kiwanda cha Tanga Fresh ndio soko kubwa la maziwa yote ya Mkoa wa Tanga na Mikoa jirani, changamoto za kiwanda hicho ni pamoja na upungufu wa mtaji na gharama kubwa za uendeshaji, Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi tayari ameshaanza majadiliano na kiwanda hicho na wadau wengine ili kutatua changamoto hizo” alisema Mhe. Kamani.

Aidha, Mhe. Kamani aliongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inatekeleza Mradi wa miaka Kumi (10) wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi(C-SDTP) katika mikoa 13 nchini (8 Tanzania Bara na 5 Zanzibar), hatua hii inalenga kuwasaidia wafugaji kwa ujumla kupata soko na bei ya uhakika ya maziwa

No comments