SERIKALI YAELEZA KUWA HAKUNA ZUIO LA KISHERIA NA KIKANUNI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MRADI WA GESI ASILIA


Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba ameliambia Bunge kuwa hakuna zuio la kisheria wala la kikanuni linalozuia utekelezaji wa mradi wa gesi asilia (LNG) wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 42, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 100. Ameeleza kuwa serikali ipo makini kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa.


Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Arif Suleman Premji, aliyetaka kujua sababu za kuchelelewa kwa mradi huo, Dkt. Nchemba amesema kinachoendelea kwa sasa ni majadiliano kati ya pande husika ili kuweka misingi imara ya utekelezaji wa mradi huo. Amesema majadiliano hayo yamefikia hatua nzuri na matarajio ni kwamba utekelezaji utaanza katika kipindi cha hivi karibuni.

Katika kulinda maslahi ya nchi, Waziri Mkuu amesema baadhi ya vipengele vinavyojadiliwa ni pamoja na kuhakikisha sehemu ya gesi inayozalishwa inatumika ndani ya nchi, pamoja na kuongeza ushiriki wa makampuni ya ndani ili kukuza uchumi wa wazawa.

Tanzania imegundua hifadhi kubwa ya gesi asilia katika mwambao wa Bahari ya Hindi, hususan katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambapo inakadiriwa kuwa na zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 (TCF) za gesi. Ugunduzi huo umeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye rasilimali kubwa ya gesi barani Afrika, huku mradi wa LNG ukitarajiwa kuongeza thamani ya rasilimali hiyo kwa maendeleo ya taifa.

No comments