SHILINGI BIL. 30.8 KUTUMIKA KWENYE CHANJO NA UTAMBUZI MIFUGO 2026/2027

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imetenga shilingi bilioni 30.8 ili kuendelea na awamu ya pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Hayo yameelezwa leo Aprili 09, 2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Mhe. Marirta Gido Kivunge lililohoji,  je serikali ina mpango gani wa kutoa huduma za dawa na chanjo muhimu ilibkuboresha afya na kuwaongezea thamani ya mifugo?

Mhe. Kamani amesema serikali inaendelea na mpango wa kudhibiti magonjwa ya mifugo kwa kutekeleza Mpango wa Chanjo na Utambuzi wa Mifugo wa miaka mitano wenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 216, unaotekelezwa kuanzia 2024/2025 hadi 2028/2029.

“Mheshimiwa Mwenyekiti katika bajeti ya Mwaka 2024/2025, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilitenga kiasi cha Shilingi Bilioni 61.2 kwa ajili kuendesha kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo, ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2026 uchanjaji umefikia asilimia 64.5 kwa nchi nzima” alisema Mhe. Kamani.

Ameongeza kuwa katika awamu ya pili ya kampeni hiyo ya chanjo, wizara imefanya tathimini ya magonjwa 13 ya kipaumbele ambayo yatazingatiwa ikiwemo Ugonjwa wa Miguu na Midomo (FMD) ambapo hadi sasa kuna aina nne vya virusi  ambavyo vimeshafanyiwa tathmini itakayosaidia kutambua aina ya chanjo itakayotumika katika eneo husika.

No comments