TANZANIA NA MISRI KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KUPITIA BANDARI YA DAR ES SALAAM



Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga,amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mheshimiwa Sherif Ismail leo tarehe 14 Aprili, 2026 katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.


Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kupitia maendeleo ya uhusiano wa kidiplomasia ya uchumi na kujadili fursa za kimkakati za ushirikiano, hususan katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na lojistiki nchini.


Majadiliano hayo yalijikita zaidi katika pendekezo la upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ambapo Serikali ya Misri imewasilisha nia yake ya kuchangia katika masuala ya usafirishaji wa meli na lojistiki za mizigo. Pande zote mbili zilisisitiza kuwa kuimarishwa kwa miundombinu hiyo kutachochea muunganiko (connectivity) bora na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za kibiashara kati ya nchi hizo mbili, jambo ambalo litaleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa pande zote.


Kupitia ushirikiano huu, Misri inalenga kutumia uzoefu wake katika sekta ya miundombinu kusaidia jitihada za Tanzania za kuwa kitovu cha biashara kikanda. Hatua hii inatarajiwa kufungua milango mipya ya uwekezaji na kuongeza ufanisi katika mnyororo wa usambazaji bidhaa ndani ya soko la Afrika, huku ikijenga misingi imara ya ukuaji wa uchumi wa viwanda kupitia mifumo ya kisasa ya uchukuzi.



No comments