TPSF YATIA SAINI HATI YA MoU NA NEPC YA BELARUS



Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limesaini rasmi Hati ya Makubaliano (MoU) na Kituo cha Taifa cha Kukuza Mauzo ya Nje (NEPC) cha Jamhuri ya Belarus, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili.


Utiaji saini huo umefanyika wakati wa ziara rasmi ya Mhe. Maxim Ryzhenkov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Belarus, aliyeambatana na Balozi Nikolai Borisevich, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kukuza Mauzo ya Nje cha Belarus (NEPC). Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, na Mhe. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb.), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ikionesha ushirikiano imara kati ya Serikali na sekta binafsi.


MoU hii inaweka mfumo wa kuimarisha mauzo ya nje, kukuza ushirikiano wa kibiashara, na kutekeleza mipango ya pamoja, ikiwemo maandalizi ya Jukwaa la Biashara la Tanzania–Belarus, linalotarajiwa kufanyika wakati wa ziara rasmi ya Mhe. Alexander Turchin, Waziri Mkuu wa Belarus baadaye mwaka 2026.


TPSF inaendelea kujizatiti katika kuendeleza ushirikiano wa kimataifa unaofungua fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania na kuimarisha ushiriki katika biashara za kimataifa.




No comments