UCHIMBAJI MCHANGA WAGEUKA KERO VIZIWAZIWA KIBAHA



Wakazi wa Sagale Magengeni, kata ya Viziwaziwa wilayani Kibaha, wamelalamikia kero ya wachimbaji mchanga wanaodaiwa kusababisha kukatika kwa barabara inayounganisha eneo hilo na Kwamfipa, hali inayowapelekea kuzunguka umbali mrefu . 


Wamesema shughuli hizo zinasababisha uharibifu wa mazingira, ikiwemo kutengenezwa kwa mashimo na madimbwi pamoja na kuharibiwa kwa baadhi ya makazi kutokana na matumizi ya magari makubwa yanayoingia na kutoka kwenye machimbo hayo.


Baadhi ya wakazi, akiwemo Hamza Duruge, Rehema Chamwene na Mwenyekiti wa Mtaa wa Sagale Magengeni, Joseph Shayo, wametoa kilio hicho wakati wa ziara ya siku ya nne ya Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Mwajuma Nyamka, iliyofanyika Aprili 13, 2026 katika kata ya Viziwaziwa.


Shayo ameeleza tayari walishachukua hatua kwa kushirikiana na maofisa mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ambao waliweka zuio la shughuli za uchimbaji mchanga, lakini bado zinaendelea kinyume cha sheria.


Baada ya mkutano wa kuwashukuru wananchi kwa kuunga mkono CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Nyamka ametembelea barabara hiyo na kuelekeza serikali ya mtaa kushirikiana na Polisi kata kuwakamata watu wanaojihusisha na uchimbaji huo haramu.


Katika hatua nyingine, Nyamka amehimiza wananchi kujitokeza kupata huduma za usajili wa vyeti vya kuzaliwa zinazotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kupitia ziara hiyo ya kata kwa kata.


Kwa upande wake, Msajili Mwandamizi kutoka RITA Kibaha, George Chuwa, alieleza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kutoa huduma katika kata nne ambazo ni Mbwawa, Visiga, Misugusugu na Viziwaziwa, sambamba na kukamilisha utoaji vyeti kwa kata ya Mbwawa na Visiga.








No comments