ULEGA AONGEZA ZAWADI UBUNIFU WA FOLENI, WENGI WAJITOKEZA
Wanafunzi wa taaluma za uhandisi wamejitokeza kwa wingi kushindana katika changamoto ya ubunifu wa kuondoa kero za foleni mijini iliyoanzishwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.
Akizungumza jijini Dodoma, Ulega alisema hadi kufikia siku ya mwisho ya wanafunzi hao kuwasilisha maandishi yao ya kitaaluma ya kupunguza foleni, maandiko 561 yamepokewa.
Waziri huyo alisema kwa ujumla, wizara na taasisi zilizo chini yake, zimetiwa moyo sana na mwitikio wa wanataluma na jamii ya Watanzania kwa ujumla, kwani imeonyesha kiu ya dhati ya kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kutumia utaalamu wa nyumbani.
Shindano hilo la ubunifu lilitangazwa na Waziri Ulega kwa mara ya kwanza Februari 23 mwaka wakati alipokuwa akizungumza na jumuiya ya wanafunzi wa taaluma za uhandisi katika ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Katika maelezo yake, Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, alisema shindano hilo litahusu wanafunzi wa taaluma za Uhandisi (Engineering), Ukadiriaji Majenzi (Quantity Surveyors), na Ubunifu Majengo (Architects).
Katika hatua nyingine, Ulega alitangaza kwamba kutokana na mwamko mkubwa uliooneshwa, zawadi kwa washindi sasa zimeongezwa kutoka katika kiwango cha awali cha shilingi milioni 10 zilizotakiwa kugawanywa kwa washindi watatu wa kwanza.
Mshindi wa kwanza atapata zawadi ya shilingi milioni 10, wa pili atapata milioni tano, wa tatu shilingi milioni tatu, wa nne shilingi milioni mbili, wa tano shilingi milioni moja huku kuanzia mshindi wa sita wa kumi wakipata shilingi laki tano kila mmoja.
Pia, Ulega alitangaza jopo la wataalamu litakalofanyia kazi mawasilisho hayo ya wasomi ambapo mshindi anatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi huu.
Post a Comment