WATENDAJI OFISI YA WAZIRI MKUU WAKUMBUSHWA KUIMARISHA WELEDI KUTIMIZA DIRA YA TAIFA 2050.

Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wamekumbushwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na kujituma ili kuhakikisha wanachangia kikamilifu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050, hususan katika maeneo ya sera, uratibu na usimamizi wa utekelezaji wake.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba  Kabudi, wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo mara baada ya kuwasili rasmi na kupokelewa na uongozi na watumjshi wa Ofisi hiyo katika Jengo la Ngome Jijini Dodoma Machi,8, 2026

Profesa Kabudi amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na ubunifu miongoni mwa watumishi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

“Ni muhimu tushirikishane mawazo na kufanya kazi kwa pamoja ili kumsaidia Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufanikisha adhima ya maendeleo yenye kuleta ustawi na furaha kwa Watanzania," amesema Profesa  Kabudi.

Aidha, Waziri Kabudi amebainisha kuwa mazingira ya kazi yenye mshikamano na mahusiano ya kifamilia hayapaswi kuwa chanzo cha uzembe au utovu wa nidhamu, bali yawe kichocheo cha kuongeza uwajibikaji na kufikia viwango vya juu vya utendaji.


Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi amewataka watumishi kuendelea kumuombea aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi hiyo, Marehemu William Vangimembe Lukuvi, ili Mwenyezi Mungu amrehemu na kumpa pumziko la milele.

“Nitaendeleza, kadri nitakavyoweza, misingi na jitihada zilizoanzishwa na mtangulizi wangu katika kuijenga Ofisi hii,” amesema.

Awali, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo,Ummy Nderiananga, amempongeza Profesa Kabudi kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kushika nafasi hiyo, akiahidi ushirikiano wa dhati kutoka kwa watumishi wote katika utekelezaji wa majukumu yake.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, naye amempongeza Waziri Kabudi kwa uteuzi huo na kusisitiza kuwa watumishi wako tayari kuongozwa na kushirikiana naye katika kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

No comments