ANZISHENI SHUGHULI ZA KUCHAKATA TAKA NGUMU KWA KUTUMIA MIKOPO YA ASILIMIA 10- PROF.SHEMDOE
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, vijana na wanawake kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri kuanzisha shughuli za ukusanyaji na uchakataji wa taka ngumu.
Profesa Shemdoe ameyasema hayo Mei 12,2026,Jijini Dodoma, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathimini ya utekelezaji wa afua ya udhibiti taka ngumu na usafi wa miji ambapo ameiasa jamii kubadili mtazamo kuhusu taka na kuona ni rasilimali inayoweza kuongeza kiuchumi na kuchangia maendeleo yao.
Amesema Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi wa taka ngumu na usafi wa mazingira nchini.
“Tumekubaliana kuwa taka ni mali, hivyo ni lazima tuziongezee thamani kwa kuanza kuzitenganisha kuanzia maeneo zinakozalishwa na tukifanya hivyo tutakuwa tumeongeza thamani ya taka na kuimarisha uchumi wa wananchi.”amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Mkoa wa Dodoma umeongeza bajeti ya usafi wa mazingira kutoka Sh milioni 750 hadi Sh bilioni 3 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambazo zitatumia pia vifaa vya usafi, kuimarisha ukusanyaji wa taka na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira.
Awali,Mwenyekiti wa wakuu wa vitengo vya udhibiti taka na usafi wa mazingira Tanzania Bara, William Mpangala kutoka Wilaya ya Bahi, aliiomba serikali kutoa maelekezo madhubuti kwa halmashauri kuhakikisha asilimia 10 ya mapato yatokanayo na udhibiti wa taka inatengwa na kurejeshwa kwenye shughuli za usafi wa mazingira.







Post a Comment