PSSSF YAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MASUALA YA HIFADHI YA JAMII
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa wa umma na wanachama kuhusu huduma, haki na wajibu unaotolewa na Mfuko huo. Mafunzo hayo ya siku mbili yalianza Agosti 17, 2026 na yalifunguliwa na Meneja wa PSSSF Kanda ya Kinondoni, Costa Mpagike, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mpagike alisema lengo la mafunzo hayo ni kujenga na kuimarisha uhusiano kati ya PSSSF na vyombo vya habari, kuongeza uelewa wa umma kuhusu shughuli za Mfuko huo, pamoja na kupunguza upotoshaji wa taarifa. “Tutawajengea uwezo ili muwe na taarifa sahihi kuhusu PSSSF na huduma zake, jambo ambalo litawarahisishia kuandika habari kwa ukweli, weledi na usahihi zaidi,” alisema Mpagike.
Mratibu wa mafunzo hayo, Nevile Meena, alisema elimu waliyoipata itawasaidia waandishi kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. “Kama hujui kitu huwezi kuandika kwa usahihi, kama unafahamu jambo utaandika kwa usahihi. Nawashukuru PSSSF kwa kutujengea uelewa. Mimi binafsi nimekuwa mwandishi wa habari wa siku nyingi lakini kuna vitu vingine nimevifahamu sasa. Kujifunza hakuna mwisho,” alisema. Naye mwandishi wa TSN, Bi. Zena Chande, alisema mafunzo hayo yamemuongezea uelewa kuhusu huduma na mafao ya PSSSF, ikiwemo kiinua mgongo na pensheni.
Kwa upande wake, mwandishi wa ITV, Julieth Robert, alisema mafunzo hayo yana tija kubwa kwa waandishi kutokana na nafasi yao ya kufikisha taarifa kwa jamii, wakiwemo wanachama wa PSSSF. Naye mwandishi wa habari mkongwe na mnufaika wa pensheni kutoka PSSSF, Beda Msimbe, alieleza umuhimu wa pensheni katika maisha yake baada ya kustaafu. “Hii pensheni inanisaidia sana katika maisha yangu ya kila siku. Sasa ni mstaafu ninayepokea pensheni kila mwezi,” alisema Bw. Msimbe.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa PSSSF wa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, hususan vyombo vya habari, katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, huduma na mafao yanayotolewa na Mfuko huo. Kupitia ushirikiano huo, PSSSF inalenga kuhakikisha taarifa zinazowafikia wanachama na wananchi zinakuwa sahihi, zenye uelewa na zinasaidia jamii kufahamu haki na wajibu wao katika hifadhi ya jamii.



.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
Post a Comment