DC MPOGOLO- AZITAKA TAASISI KUJITOKEZA KATIKA USAFI.
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa wito kwa kampuni, viwanda na taasisi zote zilizopo kando ya Barabara ya Nyerere kufika Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Taka Ngumu ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuweka mkakati wa pamoja wa kuboresha usafi wa barabara hiyo.
Mpogolo ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa zoezi la usafi lililoanzia eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi Chuo cha Utumishi wa Umma.
“Namtaka kila mmoja kuhakikisha anafika kwa mkurugenzi wetu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam au kutuma mwakilishi siku ya alhamis ili kwa pamoja tuweke mkakati wa kuhakikisha barabara yetu inakuwa safi na yenye mazingira bora,” alisema Mpogolo.
Amesema lengo la zoezi hilo ni kuhamasisha wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira pamoja na kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linaendelea kuwa safi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na mashindano ya AFCON.
Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha jiji linakuwa safi muda wote, ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa wafanyabiashara ili kuondoa biashara holela zinazochangia uchafuzi wa mazingira na msongamano wa watu na magari barabarani.
“Tunataka Dar es Salaam ibaki kuwa safi wakati wote. Ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kulinda mazingira kwa kuacha kutupa taka ovyo na kufuata utaratibu wa kufanya biashara katika maeneo yaliyotengwa,” alisema.
Aidha, amesema Serikali imeanza kutumia vyombo vya kisasa vya usafi kwa ajili ya kuondoa michanga iliyosababishwa na mvua za masika katika maeneo mbalimbali ya jiji.
“Hivi karibuni tumetoka kwenye kipindi cha mvua za masika, hivyo kumekuwa na michanga mingi barabarani. Leo tumefanikiwa kuondoa zaidi ya tani nne za michanga na taka katika maeneo mbalimbali,” alisema.
Katika zoezi hilo, wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara kandokando ya Barabara ya Nyerere walitakiwa kuhamia katika maeneo rasmi yaliyotengwa na Halmashauri ya Jiji.
Mpogolo pia aliwataka wakandarasi wa usafi kuhakikisha shughuli za usafi zinaendelea kufanyika kila siku ili kudumisha mazingira safi katika jiji hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, alisema zoezi hilo ni endelevu na wakandarasi wanaendelea kufanya usafi kila siku katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Mabelya amesema zoezi hilo ni sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani pamoja na kujiandaa na mashindano ya AFCON, huku akieleza kuwa halmashauri inaendelea kutatua changamoto ya kuziba kwa mitaro na kuondoa taka zilizozagaa katika baadhi ya maeneo kutokana na mvua za masika.
Ameomgeza kuwa matumizi ya zana za kisasa za usafishaji wa michanga barabarani yameanza kuleta matokeo chanya katika kuboresha usafi wa jiji, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na wakandarasi wa usafi katika kata zao.
“Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya tumejipanga kuhakikisha tunakuwa na zana za kisasa za usafi wa barabara. Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tunaamini zoezi hili litakuwa endelevu na kuleta matokeo chanya katika usafi wa jiji letu,” alisema.
Aidha, Mabelya amepokea miti kutoka kwa Maziku Shabani akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tabora.





Post a Comment