DKT. BASHIRU AHIMIZA KUDHIBITI UVAMIZI MASHAMBA YA MIFUGO



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amewahimiza Watendaji Wakuu wa Wizara hiyo kudhibiti uvamizi wa mashamba ya Mifugo na maeneo ya Uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi ili maeneo hayo yaweze kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya kuwa maeneo ya kuzalisha mazao ya Mifugo na Uvuvi.


Akizungumza leo Mei 9, 2026 Jijini Dodoma katika Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, Dkt. Bashiru amesema kuwa mashamba ya Mifugo yamekuwa na changamoto kubwa kiasi cha maeneo hayo kumegwa na kufanyiwa matumizi mengine bila kufuata utaratibu wa kisheria.


"siridhishwi na uvamizi wa mashamba ya Mifugo, na umegaji wa maeneo hayo ambayo yalikuwa yamepangwa kwa ajili ya shughuli za Uzalishaji Mifugo" amesema Dkt. Bashiru 


Aidha, Dkt. Bashiru amewataka Watendaji Wakuu wa Wizara kuhakikisha Sekta za Mifugo na Uvuvi zinaendeshwa Kisayansi ili kuweza kuboresha Sekta hizo ambazo ni miongoni mwa Sekta muhimu nchini.


Vilevile, Dkt. Bashiru amewapongeza Watumishi wa Wizara hiyo na Taasisi zilizopo chini yake kwa kuwa na mshikamano na uvumilivu katika kutekeleza majukumu yao ambayo yamezaa matunda katika kuendeleza Sekta zote mbili.


Pia, Dkt. Bashiru amewataka Watendaji Wakuu wa Wizara kuboresha Utendaji wao ili kufikia kiwango kile cha utendaji ambao Taasisi unapaswa kuwa nao.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Agnes Kisaka Meena, ameelezea majukumu ya Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ikiwemo na kuishauri Wizara katika kutoa huduma nzuri na bora zinazohitajika kwa wafugaji na wavuvi.


Bi. Meena, amebainisha hali halisi ya utekelezaji wa Bajeti iliyopita ambapo katika mwaka 2025/26 Wizara iliidhinishiwa kutumia shilingi Bilioni 476, na kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 111 ni matumizi ya kawaida, shilingi Bilioni 375 ni ya maendeleo ya Sekta za Mifugo na Uvuvi.





No comments