MSD, WADAU WA SEKTA YA AFYA WAJADILI MWELEKEO NA MKAKATI WA KITAIFA KUIMARISHA USALAMA WA KIFEDHA WA MNYORORO WA UGAVI WA BIDHAA ZA AFYA
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD) imeanza hatua mpya ya kimkakati ya kuimarisha usalama wa kifedha wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini, kufuatia kikao kazi kilichowakutanisha wizara ya afya, MSD na wateja wao 45 kujadili namna bora ya kuondoa na kudhibiti madeni ya taasisi zinazohudumiwa na MSD.
Akifungua kikao hicho jama Mei 13, 2026 katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu Jijini Dodoma, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, aliyoyatoa wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya MSD, Keko Mwanga, tarehe 28 Machi 2026. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dawa na Vifaa Tiba Emmanuel Tayari, alisema kuwa serikali imekusudia kuona wateja wote wa MSD wanashiriki kikamilifu katika kujenga mfumo endelevu wa kifedha utakaoihakikishia MSD uwezo wa kuendelea kutoa huduma bila kuyumba.
Naye Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi akizungumza katika kikao hicho, alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo madhubuti wa usimamizi na udhibiti wa madeni katika hospital zote zinazohudumiwa na MSD ili kuzuia kujirudia kwa changamoto ya ongezeko la madeni.
Aliongeza kuwa changamoto hiyo inapokuwa kubwa huathiri hata uwezo wa MSD kununua moja kwa moja kutoka viwandani, pamoja na kupanga akiba ya kimkakati ya bidhaa muhimu za afya, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uthabiti wa huduma za afya nchini, hususan wakati wa dharura na milipuko ya magonjwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, alisema ongezeko la madeni kutoka kwa taasisi mbalimbali limeendelea kuathiri uwezo wa bohari hiyo kutekeleza majukumu yake ya msingi, hususani katika manunuzi ya bidhaa za afya na ulipaji wa washitiri.
Akichangia mjadala, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, alisema changamoto ya madeni haiwezi kutatuliwa kwa kuangalia MSD pekee, bali inahitaji tathmini pana ya mfumo mzima wa kifedha wa sekta ya afya nchini.






Post a Comment