MWENGE WA UHURU WAZINDUA KITUO CHA AFYA LUPILA, NA MIRADI WA MAJI MAKETE
Mwenge wa Uhuru Kitaifa umekagua na kuweka jiwe la msingi leo katika Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Lupila, wenye thamani ya TZS milioni 661.
Mradi huo unajumuisha jengo la OPD, maabara, jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji na jengo la kufulia. Ujenzi umefikia asilimia 96, na kituo tayari kimeanza kutoa huduma kwa wagonjwa kutoka vijiji sita.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mbeba Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, alimpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za ujenzi wa kituo hicho pamoja na gari la kubebea wagonjwa.
Alisisitiza kuwa kiongozi huyo ana nia njema na wananchi, na aliwaasa wananchi kuendelea kumuombea pamoja na kudumisha amani na utulivu ili maendeleo yaendelee. Pia aliwapongeza viongozi wa Wilaya ya Makete kwa kusimamia ujenzi wa kituo hiki chenye hadhi ya hospitali.
Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na hatua iliyofikiwa na mradi huo.
Aidha Mwenge wa Uhuru 2026 umekagua na kuzindua leo Mradi wa Maji wa Malanduku na Kijombo uliopo Kata ya Lupila, Wilaya ya Makete.
Mradi huo wenye thamani ya TZS Milioni 904 unajumuisha tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita elfu 75. Lengo lake ni kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji vya Malanduku na Kijombo, ambao awali walikuwa wakipata shida kubwa ya maji. Sasa tatizo hilo limetatuliwa na maji yanapatikana kwa wingi.
Mwang’onda, alisema mradi umetekelezwa kwa viwango vizuri na kwa wakati. Alipongeza uongozi wa Wilaya ya Makete kwa usimamizi mzuri uliofanya mradi huu kukamilika kwa mafanikio.
Aliongeza kuwa wananchi wa Malanduku na Kijombo sasa wanafurahia matunda ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama.
Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ukiwa Wilayani Makete, umetembelea na kukagua Mradi wa Uhifadhi wa Maji katika Kata ya Ukwama, Kijiji cha Masisiwe, kwenye chanzo cha maji Itsangilawe. Pia umeshiriki zoezi la upandaji miti 200 rafiki kwa mazingira kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za wananchi za kulinda na kutunza mazingira.
“Tuendelee kupanda miti rafiki katika vyanzo vya maji. Endapo tutaona miti isiyorafiki kwenye vyanzo hivyo, tuitoe ili kuhakikisha maji yanapatikana, kwani maji ni uhai. Kila mmoja awe balozi wa kutunza vyanzo vya maji. Tutunze mazingira, nayo yatutunze.”
Aliongeza kuwa Mwenge wa Uhuru mwaka huu unasisitiza utunzaji wa mazingira. Pia aliwataka wananchi kupunguza matumizi ya mkaa na kuelekea kwenye nishati mbadala, kwani matumizi ya mkaa yanachangia uharibifu wa mazingira.
Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na hatua zinazochukuliwa na wananchi wa Makete katika kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
Kauli Mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2026:
“Tanzania Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”









Post a Comment