RAIS RUTO AHITIMISHA ZIARA YAKE YA KITAIFA NCHINI KWA MAFANIKIO, AREJEA NCHINI KWAKE



Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. William Samoei Ruto amehitimisha ziara yake ya kitaifa ya siku mbili iliyofanyika nchini kuanzia tarehe 04 hadi 05 Mei, 2026 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 


Wakati wa ziara hiyo ya kihistoria, Mhe. Rais William Ruto alipata fursa ya kuzungumza na mwenyeji wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kimkakati kama biashara, uwekezaji, nishati na uhusiano wa kindugu wa wananchi wa mataifa haya.


Kadhalika, wakati wa ziara hiyo, mikataba nane ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali ilisainiwa.


Mhe. Rais William Ruto pia alipata fursa ya kuhutubia Bunge la Tanzania jijini Dodoma, fursa aliyoitumia kuhamasisha umoja na mshikamano kwa maslahi mapana ya Tanzania  na Kenya na Kanda ya Afrika Mashariki kwa ujumla. 


Akiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma kurejea nchini kwake, Mhe. Rais Ruto alisindikizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse, Balozi wa Kenya hapa nchini, Mhe. Catherine Karemu, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ali Bujiku na Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.



















No comments