TANZANIA NA GUINEA KUSHIRIKIANA KIMKAKATI KUKUZA UCHUMI
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi ya Guinea ili kuwezesha nchi hizo kupiga hatua zaidi za maendeleo katika sekta za miundombinu, upatikanaji wa mitaji pamoja na kuvutia sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi kwa njia ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Mhe. Balozi Omar alibainisha hayo alipokutana na Waziri wa Fedha wa Guinea, Mhe. Mariama Cire Sylla, kwa lengo la kufanya mazungumzo na kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Tanzania iko tayari kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano na nchi hiyo katika maeneo ya usimamizi wa fedha za umma, ukusanyaji wa mapato, maendeleo ya viwanda, biashara, sekta ya madini, kilimo, uwekezaji na uendelezaji wa miundombinu.
‘‘Kuna maeneo Tanzania imefanikiwa ikiwemo katika utekelezaji wa miradi ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ikiwemo mradi wa MwendoKasi (BRT) pamoja na kudumisha ushirikiano na taasisi za kifedha za kimataifa jambo ambalo huongeza uaminifu wa wawekezaji na kurahisisha upatikanaji wa ufadhili wa kimataifa,’’ alisema Mhe. Balozi Omar.
Alisema kasi ya ongezeko la watu katika nchi za Tanzania na Guinea inalazimu uchumi wa nchi hizo kukua kwa kasi zaidi ili kutengeneza nafasi za kazi, kuboresha miundombinu na kuimarisha huduma za kijamii ili kuinua hali ya maisha ya wananchi.
‘‘Tanzania imebadili sera za ndani hasa katika usimamizi wa rasilimali za madini kama vile dhahabu na chuma kwa kuongeza thamani ndani ya nchi tangu mwaka 2018 badala ya kusafirisha malighafi ili kujenga na kuimarisha viwanda nchini, kutengeneza ajira za kutosha, na kuongeza mapato ya Taifa’’, alifafanua Mhe. Balozi Omar.
Aliongeza kuwa kutokana na mchango wa sekta ya kilimo na viwanda katika kuchangia pato la Taifa kwa nchi zote mbili, kuna fursa kubwa ya kubadilishana uzoefu katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na ujenzi wa sekta imara ya viwanda ili kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi.
Mhe. Balozi Omar alisisitiza kuwa ushirikiano wa Tanzania na Guinea na nchi nyingine za Afrika utawezesha kukuza sekta za ndani na kulinda rasilimali za bara hivyo kuiwezesha afrika kupiga hatua kuelekea maendeleo endelevu.
Naye Waziri wa Fedha wa Guinea, Mhe. Mariama Cire Sylla, aliipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga katika kusimamia na kukuza uchumi wake licha ya changamoto mbalimbali zinazoikanili dunia na kuathiri uchumi wa nchi nyingi barani Afrika.
Alisema kuwa nchi yake ina la kujifunza katika eneo hilo na kuahidi kuwa Guinea, itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania unaozingatia kujifunza kwa pamoja, ubadilishanaji wa utaalamu ili kuchochea maendeleo ya nchi zetu zote mbili.
‘‘Kila nchi ina maeneo ambayo kuna nafasi ya kufanya maboresho, kuna fursa kubwa ya ushirikiano katika usimamizi wa madeni na uchanganuzi wa uimara wa madeni kwani mahali ambapo Guinea imeendeleza utaalamu, Tanzania inaweza kujifunza kutokana na uzoefu wenu, na mahali ambapo Tanzania imejenga taasisi imara, sisi pia tuko tayari kushiriki maarifa na uzoefu wetu wa vitendo’’ alisema Mhe. Sylla.
Aliongeza kuwa ubadilishanaji wa wataalamu kati ya nchi hizo mbili utasaidia kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika nchi hizo katika kuboresha miongozo ya usimamizi wa madeni ili kujenga uaminifu miongoni mwa wawekezaji na kuongeza wigo wa vyanzo vya ufadhili vya kimataifa.
Mhe. Sylla alibainisha kuwa nchi yake iko tayari kujifunza kwa Tanzania namna bora ya usimamiaji wa miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, ushirikiano na taasisi za kimataifa pamoja na usimamizi wa sekta za ndani za uchumi ili kuiwezesha nchi hiyo kukuza uchumi wake kwa kasi zaidi.
Pande zote mbili zilikubaliana kuandaa mfumo rasmi wa ushirikiano kwa kushirikiana na Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa nchi hizo, utakaowezesha wataalamu kutoka nchi hizo mbili kufanya kazi kwa karibu, kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo wa kitaasisi kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi wa pande zote.





Post a Comment