UHIFADHI WA MAZINGIRA UNAHITAJI VITENDO -WAZIRI MASAUNI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Hamad Masauni amesema uhifadhi wa mazingira hauwezi kufanikiwa kwa kauli au sera pekee, bali kwa vitendo vinavyoonekana kama upandaji na utunzaji wa miti.
Masauni amesema hayo Mei 15, 2026 wilayani Kilosa mkoani Morogoro wakati wa zoezi la upandaji miti kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika Juni 5 mwaka huu mkoani Dodoma.
Amesema Dira ya Taifa ya 2050 inatambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, amesema athari za mafuriko, ukame na hali ya hewa isiyotabirika zinaendelea kuathiri maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Masauni amesisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kushiriki katika utunzaji wa mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Pia ameipongeza Wilaya ya Kilosa kwa kuwashirikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika kampeni za upandaji miti.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Balozi Baraka Luvanda amesema zaidi ya miti elfu 40 tayari imepandwa mkoani Morogoro kupitia zoezi hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema wilaya hiyo imelenga kupanda miti milioni 1.5 ili kusaidia kudhibiti mafuriko na kulinda mazingira.









Post a Comment