WCF YATOA ELIMU KUHUSU HAKI ZA FIDIA KWA WAANDISHI WA HABARI



Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi -WCF umetoa elimu kuhusu haki za fidia kwa wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo waandishi wa habari, hatua itakayoongeza uelewa wa ulinzi wa kijamii na hifadhi ya jamii nchini. 


Akizungumza katika maalum yaliofanyika jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania -TUCTA pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari wanaofanya kazi katika Vyombo vya Habari Tanzania -JOWUTA Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya amesema elimu hiyo ni muhimu katika kuwawezesha wanahabari kuelewa kwa kina masuala ya fidia kwa wafanyakazi ili waweze kuhabarisha jamii kwa usahihi zaidi. 


Amesema WCF ni taasisi muhimu inayolinda wafanyakazi wanaopata madhila kazini ikiwemo ajali, magonjwa au vifo vinavyotokana na kazi zao, hivyo ipo haja ya jamii kupewa elimu ya kutosha kuhusu huduma zinazotolewa na mfuko huo. 


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA Musa Siwayombe alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kutokana na changamoto zinazowakabili wanahabari wengi nchini, hususan ukosefu wa ajira za kudumu na mikataba isiyo rasmi katika baadhi ya vyombo vya habari. 


Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano kwa Umma wa WCF, Laura Kunenge amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wafanyakazi wanapata elimu sahihi kuhusu haki zao za fidia pamoja na huduma zinazotolewa na mfuko huo. 


Amesema waandishi wa Habari wana nafasi kubwa ya kuifikisha elimu hiyo kwa jamii kupitia vyombo vya habari, hivyo ni muhimu kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria, taratibu na mafao yanayotolewa na WCF.










No comments