FOLUR ZINGATIENI TATHMINI NA UFUATILIAJI: RAS KASKAZINI UNGUJA



Katibu Tawala wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Amir Ali Haji, ameuagiza uongozi wa Mradi wa Mifumo ya Chakula, Matumizi ya Ardhi na Urejesho wa Mandhari ya Misitu nchini Tanzania (FOLUR) kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya tathmini na ufuatiliaji. Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kufikia malengo ya mradi na kuleta tija kwa jamii. Mradi huo unatekelezwa kwa pamoja katika maeneo ya Zanzibar na Tanzania Bara.


Hayo yamesemwa wakati Mratibu wa FOLUR Kongani ya Zanzibar, Bi. Miza Suleiman Hamisi, alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi za Mkoa wa Kaskazini Unguja. Katika ziara hiyo, aliambatana na Msimamizi wa Kitengo cha Jinsia, Usalama wa Mazingira na Jamii wa mradi huo, Bw. Revocatus Kadoshi. Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa kuutambulisha mradi huo kwa Katibu Tawala huyo ambaye ameteuliwa hivi karibuni.


Katibu Tawala alitumia fursa hiyo kuzishukuru Serikali zote mbili (ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar) kwa kutambua umuhimu wa mradi huo. Alibainisha kuwa mradi una lengo la kuwepo kwa hifadhi endelevu za misitu ambazo zinalinda usalama wa chakula na kuzingatia matumizi bora ya ardhi.


"Tunapokuwa na matumizi bora ya ardhi, itatusaidia kupanga mipango endelevu yenye tija kwa jamii. Hii ni pamoja na kutunza vyanzo vya maji, kutatua changamoto ya uhaba wa chakula, na kukuza kipato cha kaya moja moja na taifa kwa ujumla," alisema Katibu Tawala.


Katika hatua nyingine Afisa Ugani wa Mradi wa Folur , Bi. Salma Kombo na Mhandisi wa Kilimo cha Umwagiliaji, Bi. Salama Yussuf wametoa mafunzo mafunzo maalum kwa viongozi wa serikali za  shehia  za Donge kipange, Pale, Mto wa Pwani na Mkokotoni  katika Wilaya ya Kaskazini B visiwani Zanzibar. 


Mafunzo hayo yenye lengo la kuzifahamisha kamati za uongozi wa Shahia kuhusu umuhimu wa masuala ya Jinsia, usalama wa mazingira na jamii pamoja nakuzifahamisha namna ya kuwasilisha kero na malalamiko ya jamii yanayoweze kujitokeza kutokana namna shughuli mbalimbali za mradi zinavyotekelezwa.




No comments