MHE. BALOZI OMAR AONGOZA VIKAO VYA KAMATI YA KUMSHAURI KUHUSU SERA ZA KODI- THINK TANK
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amefanya vikao vya Kamati ya Kumshauri (Think Tank Committees) kuhusu Sera za Kodi kilichojumuisha Serikali na Wadau kutoka Sekta Binafsi, leo tarehe 5 Juni, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage (Treasury Square), Jijini Dodoma.
Kupitia Vikao hivyo ilielezwa kuwa Serikali imepokea jumla ya mapendekezo 727 kutoka kwa wadau wa Serikali na kutoka sekta binafsi kuhusu Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Ada na Tozo mbalimbali yalipokelewa na kuchakatwa ikiwa ni mojawapo ya maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2026/2027, yakilenga kufanya maboresho kwenye Sheria na Kanuni mbalimbali za kodi, ada na tozo.
Hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali ni muhimu katika kutekeleza dhana nzima ya uwazi na kuishirikisha jamii nzima katika uandaaji wa Bajeti ya Seikali na kama njia moja wapi ya kuchochea na kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini yanayolenga kukuza zaidi uchumi na ustawi wa jamii.
Katika vikao hivyo, Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa mkakati wa Serikali ni kukuza uchumi, kuhamasisha uwekezaji na kukuza sekta ya viwanda vya ndani, na kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo kutekeleza Bajeti yake ambapo katika Mwaka ujao wa Fedha, Serikali imekusudia kuitekeleza kwa kutumia mapato yake ya ndani kwa zaidi ya asilimia 75.
Kikao hicho pia kimeishirikisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiongozwa na Waziri wake wa Fedha na Mipango, Mhe. Alhaji Dkt. Juma Malik Akil.











Post a Comment