SAYANSI NA UBUNIFU KUONGEZA KASI YA TANZANIA KUSHINDANA KIUCHUMI DUNIANI



Tanzania imetajwa inatazamiwa kuwa nchi yenye uwezo mkubwa wa kubadilisha matokeo ya tafiti za kisayansi kuwa bidhaa zenye thamani ya kiuchumi kupitia uwekezaji katika ubunifu, teknolojia na tafiti za afya.


Hayo yameelezwa leo Juni 09, 2026 na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika Kongamano la 33 la Kisayansi la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC jijini Arusha ambapo imebainishwa tayari NIMR imefanikiwa kufanya ugunduzi na uzalishaji wa dawa za asili kutoka mimea tiba huku baadhi ya dawa na bidhaa za lishe zikiwa zimeingia sokoni.


Amesema mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa Tanzania inaweza kubadilisha tafiti kuwa bidhaa na huduma zinazochochea ukuaji wa uchumi pamoja na ustawi wa wananchi.


“Hii ndiyo maana halisi ya Research Commercialization. Tunataka kuona matokeo ya tafiti yakitoka maabara na kufika sokoni. Tunataka kuona safari kamili kutoka ugunduzi hadi uwekezaji, kutoka wazo hadi kiwanda na kutoka tafiti hadi ustawi wa wananchi,” amesema Mhe. Mchengerwa.


Mhe. Mchengerwa ameongeza mabadiliko ya teknolojia kwenye dunia ya sasa yanakuza ushindani mkubwa unaotokana na maarifa, ubunifu na teknolojia, hali inayozifanya nchi zinazowekeza katika sayansi na ubunifu kuwa na nafasi kubwa ya kuongoza uchumi wa baadaye.


Aidha, Serikali imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kama nyenzo muhimu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikielezwa kuwa afya ni msingi wa maendeleo ya uchumi, tija na ustawi wa Taifa.









No comments