SERIKALI YAJA NA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA



Serikali imeandaa mikakati mbalimbali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira ili kufikia azma ya kuwa na Tanzania ya kijani ifikapo mwaka 2050.


Akizungumza leo Juni 5, 2026, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema Tanzania inatarajiwa kuwa na watu milioni 118 ifikapo mwaka 2050, jambo litakaloongeza mahitaji ya rasilimali muhimu zinazotegemea mazingira salama na endelevu.


“Ongezeko hili la watu litahitaji rasilimali za maji, ardhi yenye rutuba na mazingira bora. Hili linapaswa kutukumbusha wajibu wetu wa kutunza mazingira na kuimarisha usimamizi wake. Natoa maagizo kwa mamlaka zote za serikali za mitaa nchini kuongeza usimamizi wa mazingira kwa kuandaa bustani na kuhakikisha vibali vya ujenzi vinazingatia sharti la upandaji wa miti angalau mitano. Aidha, nawasihi wadau na wananchi wote kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira,” amesema Dkt. Nchimbi.


Aidha, amesema serikali imejipanga kuongeza mapato ya taifa kupitia biashara ya kaboni na kuagiza mamlaka za serikali za mitaa kubainisha na kusajili maeneo ya misitu yatakayoweza kutumika katika shughuli za biashara hiyo.


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yenye changamoto za uharibifu wa mazingira pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira.


Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha taifa linaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira.


Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira mwaka 2026 yalianza Juni 1 na kuhitimishwa Juni 5, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “DIRA 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”


Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilishiriki pamoja na taasisi zake kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa ajili ya kuendeleza shughuli za ufugaji na uvuvi wenye tija na endelevu.

No comments