SERIKALI YAZINDUA KITUO CHA OPERESHENI NA MAWASILIANO YA DHARURA MWANZA



SERIKALI imezindua rasmi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura cha Mkoa wa Mwanza, hatua inayolenga kuimarisha uratibu wa shughuli za usimamizi wa maafa na majanga katika mkoa huo.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Juni 5, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda, amesema kituo hicho ni nyenzo muhimu katika kufuatilia na kudhibiti matukio ya dharura kwa ufanisi zaidi na mkoa unaweza kufuatilia matukio ya dharura kwa karibu, kukusanya na kuchambua taarifa kwa wakati pamoja na kuimarisha mawasiliano kati ya wadau mbalimbali wa usimamizi wa maafa.


Hatua hiyo amesema ni sehemu ya jitihada za serikali kujenga mfumo jumuishi wa usimamizi wa maafa wenye uwezo wa kutoa mwitikio wa haraka na wenye ufanisi katika kukabiliana na majanga hivyo kuwataka watumishi na viongozi kutumia mafunzo wanayopata kujenga uelewa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano wa kiutendaji ili kuboresha zaidi usimamizi wa maafa katika Mkoa wa Mwanza.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, amesema kituo hicho kinakuwa kitovu cha ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa taarifa za matukio ya dharura na maafa, ambapo kinaunganishwa moja kwa moja na Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, hivyo kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kufanya maamuzi ya haraka na sahihi.


“Kupitia kituo hiki, Serikali inaweza kufuatilia vihatarishi mbalimbali, kutoa tahadhari za mapema, kuratibu rasilimali za kukabiliana na maafa na kuimarisha mawasiliano kati ya wadau wote wanaohusika na usimamizi wa maafa,”amesema.








No comments