TWANGE: UZALISHAJI UMEME NCHINI NI IMARA LICHA YA HITILAFU YA GRIDI YA TAIFA

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema hali ya uzalishaji wa umeme nchini inaendelea kuwa imara licha ya hitilafu iliyojitokeza kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa Juni 27, 2026 na kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Twange amesema uwezo wa uzalishaji wa umeme umefikia takribani megawati 4,400, kiwango kinachokidhi mahitaji ya sasa ya nchi, huku akisisitiza kuwa tukio hilo halikutokana na upungufu wa uzalishaji wa umeme.


Amefafanua kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha hitilafu hiyo ilisababishwa na matatizo yaliyojitokeza kwa wakati mmoja katika njia tatu za usafirishaji wa umeme pamoja na mashine moja ya kuzalisha umeme, hali iliyoathiri Mfumo wa Gridi ya Taifa.


Twange ameeleza kuwa Gridi ya Umeme ya Taifa ni mfumo mmoja unaounganisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, hivyo hitilafu kubwa katika sehemu moja inaweza kuathiri mfumo mzima na kusababisha kukatika kwa umeme katika maeneo mengi kwa wakati mmoja.


Aidha, amewaomba radhi wananchi na wateja wote walioathirika na tukio hilo na kuahidi kuwa TANESCO itaendelea kuimarisha miundombinu yake pamoja na kuchukua hatua za kiufundi ili kupunguza uwezekano wa kujirudia kwa hitilafu za aina hiyo siku zijazo.







No comments