VIJANA 10 BORA WA VIJANA UCHUMI CHALLENGE KUNG'AA MBELE YA RAIS SAMIA JULAI 6

 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi Julai 6 mwaka huu katika hafla ya kuwatunuku washindi 10 bora wa mashindano ya Vijana Uchumi Challenge 2025/2026, itakayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.


Akifunga kambi ya Vijana Uchumi Challenge iliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kwamfipa mkoani Pwani, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Jenifa Omolo, amesema Serikali itaendelea kuwashika mkono vijana wote 100 waliofika hatua ya kambi ili mawazo yao yawe miradi yenye tija.


Amesema hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya vijana 3,000 pamoja na wageni mbalimbali, huku akisisitiza kuwa kambi hiyo si mwisho wa safari ya washiriki bali ni mwanzo wa hatua ya kuendeleza na kutekeleza mawazo yao.


Omolo ameeleza, mashindano hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwashirikisha vijana katika ujenzi wa uchumi wa taifa.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Joseph Malekela, amefafanua vijana 100 walichaguliwa kuingia kambini baada ya kuchambuliwa maombi 7,852 yaliyowasilishwa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.


Kwa niaba ya washiriki, Raiyan Juma Amour kutoka Zanzibar ameiomba Serikali kuyaendeleza mawazo yaliyowasilishwa na vijana hao ili yatumike kuleta mageuzi ya kiuchumi na kutatua changamoto mbalimbali nchini.







No comments