WASIRA: HATUFUNGAMANI NA UPANDE WOWOTE, TUNAAMUA MAMBO KWA MASLAHI YA NCHI



Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema ziara ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi inathibitisha dhamira ya Tanzania kutofungamana na upande wowote.


Akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wilayani Same mkoani Kilimanjaro Juni 9, 2026 wakati wa kuhitimisha ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, Wasira alisema waasisi wa Taifa wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere waliitaka Tanzania kukaa katikati pale pande mbili zinapogombana.


“Tulitaka tuwe huru na uhuru uwe wa kudumu. Kazi yetu ni kudumisha uhuru na kudumisha uhuru ni kutupa haki ya kuamua mambo tunayoona yanatufaa sisi, sio kutegemea wengine wakuambie mfanye nini,” alisema.


Akizungumzia maswali kuhusu ziara ya Rais Samia Urusi, Wasira alidai: “Na juzi Rais wetu ameenda Urusi wengine wanauliza ameenda kufanya nini. Mbona alivyoenda China hamkuuliza, mbona alipoenda Marekani hamkuuliza. Akienda Urusi mnaanza kuuliza ameenda kufanya nini? Ni mawazo yenu kichwani ya kufikiri Marekani au Ulaya ya Magharibi ndio wenye dunia yao, lakini dunia ni ya wote."


Aliongeza: “Sisi tangu Mwasisi wetu Nyerere alituambia ‘katika dunia inayogombana sisi tusiwe na upande’. Tukigombana Warusi na Marekani, sisi tunakaa katikati. Kwa hiyo ukienda Marekani baadae unaenda Urusi na wewe huna haja ya kuuliza tumeenda kufanya nini.”


Wasira alisisitiza kuwa CCM ilijipa kazi ya kupambana na dhuluma ndani na nje ya nchi. “Wala hatuwezi kulea dhuluma ndani ya nchi. Huo ndio uhuru tuliodai, kwa kuamua mambo yetu na kuhakikisha watu wetu wanaishi bila kudhulumiwa,” alibainisha.






No comments