JKCI NA BMH WAUNGANISHA NGUVU KUIMARISHA UTALII TIBA



Watoto kutoka nchini Burundi waliokuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), hatua inayozidi kuiimarisha Tanzania kama kitovu cha utalii tiba barani Afrika.

Upasuaji huo umefanyika kupitia kambi maalumu iliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kuonesha uwezo wa wataalamu wa Tanzania katika kutoa huduma bingwa bobezi za upasuaji wa moyo kwa watoto.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, alisema mafanikio yaliyopatikana yanaonesha uwezo wa wataalamu wa Kitanzania kutoa huduma za kibingwa kwa viwango vya kimataifa kupitia ushirikiano wa kitaalamu.

Alisema kambi hiyo pia ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya afya, hususan katika kuimarisha huduma za kibingwa na bobezi.

"Kambi hii ni mwanzo wa ushirikiano wa kudumu kati ya BMH na JKCI wenye lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za magonjwa ya moyo kwa Watanzania na wagonjwa kutoka mataifa mengine," alisema Profesa Makubi.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kwa Watoto kutoka JKCI, Dkt. Godwin Sharau, alisema ushirikiano huo umeziwezesha timu za wataalamu kubadilishana uzoefu na kuongeza uwezo wa kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto kwa ufanisi zaidi.

Naye Mratibu wa Utalii Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Asha Mahita, alisema mafanikio ya kambi hiyo yanaunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba barani Afrika.

Alibainisha kuwa kuimarika kwa huduma za kibingwa nchini kunachangia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi, huku kukivutia wagonjwa kutoka mataifa mengine kuja kupata matibabu nchini Tanzania.








No comments