SERIKALI YAHARAKISHA UTEKELEZAJI WA MRADI WA TABIANCHI NA UHIFADHI WA BIOANUWAI
Serikali imeagiza taasisi zinazotekeleza Mradi wa Integrated Net-Zero Nature-Positive Solutions for Climate and Biodiversity Protection kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli zilizobaki ili kuhakikisha mradi huo unachangia kikamilifu katika juhudi za Taifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda bioanuwai na kujenga uchumi wa kijani.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Daniel Pancras, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi wa Mradi kilichofanyika jijini Arusha.
Dkt. Abbasi amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekeleza vipaumbele vya Taifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuunganisha sekta mbalimbali ikiwemo mazingira, misitu, nishati, uchukuzi na serikali za mitaa.
Amesisitiza kuwa taasisi zote zinazoshiriki utekelezaji zinapaswa kuondoa changamoto zinazochelewesha shughuli za mradi ili matokeo yaliyokusudiwa yaweze kupatikana kwa wakati na kuleta manufaa kwa wananchi pamoja na mazingira.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dkt. Zainabu Shabani Bungwa, akisoma taarifa ya Kamishna wa Uhifadhi, amesema utekelezaji wa mradi unaendelea kuimarika kufuatia kuongezwa kwa wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Nishati katika timu ya usimamizi.
Amesema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa uratibu, kuimarisha ushirikiano wa taasisi zinazotekeleza mradi na kuhakikisha malengo ya Taifa ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu yanafikiwa.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Post a Comment