KIUNGO WA MAMELODI SUNDOWNS NA TIMU YA TAIFA YA AFRIKA KUSINI JAYDEN ADAMS AFARIKI DUNIA AKIWA NA MIAKA 25

 


Kiungo wa klabu ya Mamelodi Sundowns na timu ya taifa ya Afrika Kusini, Jayden Adams, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 25, wiki chache baada ya kuiwakilisha nchi yake katika Kombe la Dunia la 2026.

Adams alikuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi zote tatu za hatua ya makundi kwa Afrika Kusini, huku timu hiyo ikiandika historia kwa kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia kabla ya kuondolewa na wenyeji wenza Canada katika hatua ya 32 bora.

Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini, Gayton McKenzie, amesema amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Adams.

Amesema soka la Afrika Kusini limepoteza mmoja wa vipaji vyake vikubwa, huku taifa zima likiungana na familia, wachezaji wenzake na mashabiki katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Kwa mujibu wa Polisi wa Afrika Kusini, uchunguzi umeanza baada ya mwili wa mwanaume mwenye umri wa miaka 25 kupatikana ndani ya nyumba moja eneo la Schotschekloof, katikati mwa Jiji la Cape Town, Jumamosi asubuhi. Hata hivyo, chanzo cha kifo hicho bado hakijathibitishwa.

Waziri McKenzie ametoa wito kwa vyombo vya habari na umma kuepuka kutoa taarifa au kufanya uvumi kuhusu chanzo cha kifo hicho hadi uchunguzi utakapokamilika na taarifa rasmi kutolewa na mamlaka husika.

Katika Kombe la Dunia, Adams alianza katika mchezo wa sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Czech licha ya kupokea taarifa za kifo cha bibi yake saa chache kabla ya mechi kuanza.

Chama cha Wachezaji wa Soka Afrika Kusini (South African Football Players Union) kimesema kimeguswa sana na kifo cha ghafla cha Adams, kikieleza kuwa alikuwa ameibeba bendera ya taifa kwa heshima, ujasiri na kujituma katika Kombe la Dunia la 2026.

Adams alianza maisha yake ya soka akiwa Stellenbosch FC kabla ya kujiunga na Mamelodi Sundowns Januari mwaka 2025, ambako alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Afrika Kusini kilichofika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2024 kabla ya kuitwa katika kikosi cha kocha Hugo Broos kwa ajili ya Kombe la Dunia, ambapo Bafana Bafana waliandika historia kwa kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza.

No comments