SERIKALI YAWEKEZA TIBA YA MICHEZO KUELEKEA AFCON 2027


Serikali imeanza maandalizi ya kuimarisha huduma za tiba ya michezo kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kupitia uwekezaji wa jengo maalumu litakalojengwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika tawi lake la Temeke.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuimarisha huduma za afya za kibingwa na kuweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuhudumia wanamichezo wa ndani na wa kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Tawi la JKCI lililopo Hospitali ya Dar Group, Tazara jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema uwekezaji huo unakwenda sambamba na maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON 2027.

Profesa Mkumbo alisema pamoja na kuimarisha huduma za tiba ya michezo, JKCI imeendelea kuokoa fedha za Serikali kwa kutoa huduma za kibingwa nchini, ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita taasisi hiyo imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 37 ambazo hapo awali zilitumika kuwapeleka wagonjwa wa moyo nje ya nchi kwa matibabu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, alisema jengo hilo litatoa huduma za uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa afya za wanamichezo, hatua itakayoongeza utayari wa sekta ya afya kuelekea mashindano ya AFCON 2027.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, alisema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 18 utaongeza uwezo wa taasisi hiyo kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika tiba ya moyo, tiba ya michezo na huduma nyingine maalumu kwa viwango vya kimataifa.

Alisema uwekezaji huo pia utaimarisha utalii tiba na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uwezo wa kutoa huduma maalumu za afya kwa wagonjwa na wanamichezo kutoka ndani na nje ya nchi.







 

No comments